October 23, 2010

TWIGA STARS YAELEKEA SOUTH AFRICA

Twiga stars timu ya mpira wa miguu ya wanawake yaelekea South Africa. Timu hiyo itapita Botswana kwaajili ya kucheza mechi mbili kujipima nguvu. Watanzania wote tuwaunge mkono, tuwaombee dua warudi na ushindi wa kishindo. Tanzania nasi tunaweza!
 Twiga Stars itaikabili Banyana Banyana ya Afrika Kusini Oktoba 31, siku ambayo Watanzania watakuwa wakipiga kura kuchagua viongozi wao.

Twiga Stars watacheza mchezo huo wa ufunguzi wa michuano hiyo ya soka ya wanawake ya Afrika, wakiwa Kundi A ambalo linazo pia timu za Nigeria na Mali.

Kocha wa timu hiyo, Boniface Mkwasa alisema  jana kuwa watakosa haki yao ya msingi kama Watanzania ya kupiga kura, lakini watakuwa katika jukumu lingine la kuiwakilisha nchi yao katika fainali hizo, jambo  ambalo linawafariji.

Mchezo wa Twiga Stars na Banyana  utachezwa kwenye Uwanja wa Sinaba mjini Joharnesburg.

Akizungumza na Mwananchi  baada ya mazoezi yao  jana asubuhi ,  Mkwasa alisema wanasikitika kukosa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka kutokana na kuwa na jukumu hilo na hawawezi kuacha kushiriki fainali hizo kwani tayari ratiba imetolewa.

Alisema mbali ya kukosa nafasi hiyo kwa sasa wanaelekeza nguvu zao katika mchezo huo kwani macho na masikio ya Watanzania yatakuwa kwao, hivyo watahakikisha wanatumia vyema nafasi yao kwa nia ya kuilinda na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

"Ni kweli tunacheza siku ambayo taifa letu litakuwa katika shughuli ya upigaji kura na sisi kama Watanzania ambao tuna kila sababu ya kushiriki hatutaweza kufanya hivyo kutokana na kuwa na jukumu hilo,"alisema Mkwasa.

Alisema,"kikubwa kwa sasa wachezaji waelekeze nguvu zao katika fainali hizo wasiangalie masuala ya siasa kwani ratiba haiwezi kubadilishwa, hivyo sisi tutakuwa na jukumu lingine wakati wenzetu wakipiga kura."

Aidha Mkwasa alisema maandalizi kwa ajili ya safari yao yanakwenda vizuri na kwa sasa wameliachia shirikisho la soka nchini, TFF kuhusu safari yao na ameongeza kuwa endapo ratiba itakwenda kama ilivyopangwa watacheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kuelekea Afrika Kusini.

Timu hiyo itaondoka nchini Jumapili ambapo kabla ya kuwasili Afrika Kusini itacheza na Zimbabwe pamoja na Swaziland michezo ya kirafiki ili kujiweka fiti zaidi.

Wakati huo huo, kocha wa timu ya wanawake ya Nigeria 'Super Falcon', Eucharia Uche anatarajia kutangaza kikosi cha wachezaji 21 kesho ambao wanatoka katika timu za U-17 na U-20 ambao watacheza dhidi ya Twiga Stars katika michuano hiyo.

"Nimeona wachezaji wazuri na wenye uwezo ambao wanatoka kwenye timu za vijana (U-20) na wataweza kutengeneza timu nzuri na ni matumaini yangu nilivyowaona katika mazoezi watasaidia kwa kiasi kikubwa katika uteuzi wangu wa mwisho na kila kitu kinakwenda vizuri kwa upande wa maandalizi na tuko tayari kwa fainali hizo,"alisema kocha huyo.


No comments:

Post a Comment