October 22, 2010

Rooney akalia kuti kavu Man United

<>
LONDON, Uingereza
MSHAMBULIAJI Wayne Rooney anakabiliwa na hatari ya kuondolewa kikosi cha kwanza cha Manchester United  baada ya kumkosoa kocha wake, Alex Ferguson.

Kutokana na kauli yake akipingana na Ferguson kwamba hakuwa majeruhi, sasa ni dhahiri Rooney anaweza kuachwa benchi kwenye mchezo wa leo dhidi ya West Brom.

Rooney, pia alimhoji kocha wake kwanini ameachwa benchi katika mechi mbili ilizocheza klabu hiyo.

Ferguson alisema  Rooney aliachwa benchi dhidi yaValencia na Sunderland kutokana na kuwa majeruhi wa kano ya goti, akidai kwamba mshambuliaji wake huyo aliwaficha madaktari wa klabu kuhusu ukubwa wa maumivu yake

Lakini, baada ya mechi ambayo England ilitoka suluhu 0-0 dhidi ya Montenegro  Jumanne,  Rooney alikana madai ya kocha wake.

Madai yake yaliungwa mkono na daktari wa timu ya taifa, Gary Lewin, ambaye alieleza:
"Ninachoweza kuzungumzia ni siku saba ambazo Wayne alikuwa kikosi cha England, alifanya mazoezi kila siku  na alikuwa fiti kwa mchezo.

"Ni kweli kwamba hajaichezea Man  United  kwa wiki mbili kabla ya mechi ya England na kilichotokea kwenye klabu yake (United ) ni  kati yake na kocha wake . Lakini, alipowasili hapa, alikuwa fiti na tayari kufanya mazoezi na kucheza."

Ferguson huenda alikuwa akimpumzisha na kumwepusha na kufuatiliwa mno na vyombo vya habari  na maisha yake binafsi, lakini sina shaka Rooney  alitaka kucheza."

Kocha huyo alikuwa na imani kuwa baada ya kumpumzisha, kisha mchezo ambao ulidhaniwa ungekuwa rahisi ya Montenegro,  Rooney angekuwa tayari kuikabili Brom leo kwenye Uwanja wa  Old Trafford.

Lakini, baada ya kurejea Rooney  alionyesha mchezo dhaifu kwenye Uwanja wa Wembley kiasi cha kuzomewa yeye na wenzake.

Kwa sababu hiyo, Ferguson anaweza kumuadhibu kwa kuonyesha utovu wa nidhamu na ukaidi.

Kimsingi, anaweza kumwacha kwa madai kwamba hana kiwango kizuri cha kucheza leo.

Rooney,   25, hajafunga bao lolote kwa Man United tangu  Machi, ingawa msimu huu amefunga moja kwa penalti.

Man United imekuwa na mpango wa kumpa mkataba mpya wa miaka mitano.

Lakini, kuna shaka kwamba huenda asisaini huku Real Madrid ikisubiri kwa hamu kumnyakua.

No comments:

Post a Comment